Inakuwaje Watanzania wenzangu na wapenda burudani? Mimi niko poa ile mbaya, naendelea kuwadondoshea ishu za ukweli kupitia hapa EBWANADAAH, blog yenu yenye kila aina ya za raha a.k.a burudani zinazoendelea kufanyika kila kukicha.
Mwishoni mwa wiki iliyopita macho na masikio ya Wabongo wengi vilikuwa pale ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee zilipofanyika sherehe za utoaji tunzo kwa wasanii wa muziki, watayarishaji video, muziki na wadau wengine wa sanaa hiyo waliyofanya vyema msimu uliyopita yaani 2010-2011.
Mimi pia nilikuwa ni miongoni mwa wadau wa burudani waliyokuwa makini kufuatilia kila 'kategori' ili kufahamu nani na nani watatunzwa baada ya kufanya vizuri mwaka jana ili nikufahamishe wewe mpenzi wa blog hii ambaye hukupata nafasi ya kuzicheki sherehe hizo kwa kuzama ukumbini au kupitia luninga yako a.k.a kitu cha live.
Najua wengine watakuwa wameshaanza kusahau kilichotokea siku hiyo na kuamua kuendelea na mishemishe za kusaka mkwanja huku wakibaki na viulizo kichwani kuhusiana na udhaifu uliyojitokeza siku hiyo. Lakini kwa kijana wa 'Farm Boyz' ya kule Kimanzichana, Habas Hamisi Kinzasa a.k.a 20% bado ni furaha kwa kwenda mbele na inawezekana asiisahau siku hiyo iliyompatia tunzo 5 za halali, zisizokuwa na skendo hata moja.
Ukweli ni kwamba, kila penye zuri, baya huwa linatafuta nafasi ya kujipenyeza na kutia dosari hata kidogo ili ishu nzima ionekana haikuwa poa. Binasfi nakiri kwamba, waandaaji wanastahili pongezi kubwa kwa kufanikisha kila kitu mpaka tunzo hizo kutua mikononi mwa wahusika, waswahili wanasema kuwa siku zote huwa hakuna shughuli ndogo hata kama ni arobaini ya kumtoa mtoto nje. Hivyo ninayo kila sababu ya kutoa 'rispekti' kwa Kilimanjaro na wote waliyofanikisha hilo, likiwemo Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Lakini pamoja na pongezi hizo pia sitokuwa mnafiki kwa kuweka bayana yale machache yaliyozifanya sherehe hizo ziingie dosari. Kwakuwa mimi ni miongoni mwa wadau wa sanaa ya muziki nchini napenda tunzo hizo ziendelee kuwepo na kuwa bora zaidi kwani zinaleta changamoto kwa wasanii na tasnia nzima ya game hiyo Bongo kwani nikifunga domo langu sitohusika kwa namna moja ama nyingine katika kuziboresha, zaidi nafsi yangu itakuwa inanisuta.
Kama wewe msomaji haufahamu, yamekuwepo malalamiko kutoka baadhi ya wasanii wanaofanya maisha yao mikoani ambao majina yao yalitajwa kuwania tunzo hizo. Mmoja wa wasanii hao aliyepiga stori na Ebwanadaah ni Jetman anayeishi Harusha ambaye ngoma yake ilitajwa kuwania Tunzo ya wimbo Bora wa Ragga Dancehall, alisema kuwa alisikitishwa na kitendo cha waandaaji kutowajali wasanii wa mikoani waliyotajwa kuwania tunzo.
"Sijajua hizo tunzo zinaendeshwa kwa staili gani au zinawahusu wasanii wa Dar peke yao? Mimi nilishangaa kutoshirikishwa kwa chochote wakati wimbo wangu umeingizwa kwenye shindano. Wao kama waandaaji walitakiwa wawasiliane na mimi tangu kazi yangu ilipoingizwa, lakini mpaka zinakaribia fainali nilikuwa sijui chochote kinachoendelea, nikajaribu kupiga simu kwa wahusika ili nijue nitawezaje kushiriki katika sherehe hizo lakini wakawa hawapatikani na walipopatikana hawakupokea. Ninavyofahamu mimi msanii yoyote anayetajwa kuwania tunzo lazima awepo siku ya tukio ili kama atashinda akabidhiwe labda kama atakuwa na dharula ya muhimu, lakini Kibongo naona vinafanyika vitu kienyeji sana," alisema Jetman a.k.a Dizano anayefanya muziki wa 'dancehall'.
Ukweli ni kwamba, waandaaji wanatakiwa wawe wanajitahidi kuhakikisha kila msanii ambaye kazi yake imetajwa kuwania tunzo hizo anakuwepo ili kuepuka ile hali ya nani akamchukulie fulani kama ilivyotokea kwenye kategori ya Msanii Bora wa kike ambapo Lady Jaydee alichukuliwa tunzo yake na shabiki baada ya kimya cha muda na watu kusubiri huenda Jide ataibukia kona fulani ya ukumbi lakini wapi, wala haikuelezwa sababu za yeye kutokuwepo kama ilivyokuwa mwaka jana ambapo mumewe Gadner alipomtetea kwamba ameshindwa kuhudhuria kwenye tunzo hizo kwasababu alikuwa na kazi katika ukumbi mmoja wa burudani, hivyo aliheshimu mkataba wake.
Vivyo hivyo katika Wimbo Bora wa Afrika Mashariki, kama tumeamua kwenda Kiafrika Mashariki basi siyo mbaya wasanii hao wakipewa mualiko ili kama wanashinda wakabidhiwe tunzo zao, lakini siku hiyo Kidumu kutoka Kenya sikumuona na haikutajwa sababu yoyote ya yeye kutokuwepo zaidi ya kuchukuliwa tunzo yake na shabiki. Mbona sisi huwa tunazifuata zile za Kisima kule Kenya, Parm (Uganda), MTV Afrika, Channel O, Kora na nyingine ambazo huwa zinatuhusu. Amini nawaambia kwa kufanya hivyo heshima kubwa itashuka kunako tunzo hizo. Kingine ni kwamba ile shoo kali mliyotuahidi kutoka kwa wasanii wetu wa nyumbani ambao mliwalipa vizuri mbona sikuiona? Nilichokiona mimi ni kile nilichokizoea siku zote ambacho sikuhitaji kukitia machoni tena, kwani wasanii ni wale wale na nyimbo ni zile zile.
Mimi kama mdau wa burudani nauliza kwamba; Hivi Tanzania haina wasanii wapya wanaofanya vizuri ambao watu wanahitaji kuwaona jukwaani, kama hawapo mbona kwenye kategori zenu zipo za wasanii chipukizi? Kama mlikuwa hamjui Wabongo wengi nikiwemo mimi tunahitaji vitu vipya kila siku na siyo shoo zile tulizozoea za mtu mmoja kusimama jukwaani na kupiga kelele kisha anashuka, anatia mkwanja wake mfukoni anasepa. Nilitegemea kuona wasanii kama Linex, Sam wa Ukweli, Ben Paul, Beka, Ditto, Mataluma, Dogo Janja, Godzilla, Belle 9 na wengine wengi wanaofanya vyema hivi sasa wanapata nafasi ya 'kupafomu' stejini.
Pia zamani sheree hizo zilikuwa zinapambwa na ngoma za asili kutoka katika vikundi mbalimbali akiwemo Wanne Star, lakini siku hizi ni muziki wa kizazi unachukua nafasi kubwa, ambao kwa jinsi wasanii wetu wanavyofanya unaonekana hauna mvuto jukwaani. Kama hamuamini hilo mnakumbuka mashabiki walivyowapokea kina Banana walipoimba wimbo wa Msondo, Binadamu tumeumbwa mateso? Msifikiri wote wanaokuja pale wanapenda Hip Hop. Yapo matatizo mengine mengi ambayo kama hayatorekebishwa yatazifanya tunzo hizo zizidi kupoteza mwelekeo kila mwaka, inawezekana siyo makosa ya waandaaji bali ni ya wale wanaojiita wadau ambao wanapopata nafasi ya kushiriki kufanikisha shughuli hiyo huitumia vibaya, pengine kwa kutokwa na uelewa kuhusu sanaa ya muziki au kujisahau. Ni hayo tu.
Wenu katika kuboresha tunzo hizo.
MC George.
0715 110 173
One Responses to "NILICHOKIONA TUNZO ZA KILI 2010-2011"