"Napenda kuwa na mke mwenye heshima na adabu wakati wote na asie na ubaguzi hata kidogo na mwenye kuendana nami"
Kijana toka pande za Sinza ambaye anapiga kazi ndani ya kundi la TMK Wanaume Family, Saidi Juma Hassan a.k.a Chegge Chigunda, Mtoto wa Mama Said ndiye staa aliyetiliwa maguu na Mpaka Home na kuangusha naye stori kibao kuhusiana na maisha yake hasa nje ya muziki.
Kama tulivyomtambulisha hapo juu, Sinza Madukani, Dar es Salaam ndiyo sehemu anayofanya maisha yake. Majira ya mchana, wiki iliyopita Mpaka Home ilikuwa kwa mchizi ambaye amepanga kunako gheto moja la kiushikaji. Shuka chini ili ujue mengi zaidi kuhusu maisha yake.
Mpaka Home: Inakuwaje Chegge, siku zote nilikuwa nadhani unaishi Temeke, lini umehamia Sinza?
Chegge: (Kicheko kidogo) mimi miaka yote ya maisha yangu huwa naishi Sinza, hata familia yangu karibu yote ipo jirani tu kutoka hapa.
Mpaka Home: Je, unaishi vipi na majirani zako?
Chegge: Niko nao vizuri sana, tena wananipenda ile kichizi mtu wangu, sijawahi kusikia tuhuma hata moja ya kuniponda kutoka kwa majirani zangu hata machizi wangu wote wa kitaa.
Mpaka Home: Kitu gani usichokipenda katika maisha yako?
Chegge: Nawachukia sana watu wanaopenda kukwamisha maendeleo yangu na wezi wa kazi zetu kwa ujumla.
Mpaka Home: Unadhani lini utakuwa na mjengo wako na kuepukana na adha ya kupanga?
Chegge: Siku yoyote, hiyo mipango ipo naamini Mungu ndiye mpaji.
Mpaka Home: Unalionaje shindano lako la kutafuta mke linaloendelea katika gazeti hili?
Chegge: Nadhani litanisaidia kwa kuwa matarajio yangu baadaye ni kuwa na mke na ningependa Mpaka Home iwe ya kwanza kulijua jambo hilo.
Mpaka Home: Ungependa kuwa na mke mwenye tabia zipi?
Chegge: Napenda mwanamke yoyote mwenye heshima na adabu wakati wote na asiye na ubaguzi hata kidogo na mwenye kuendana nami.
Mpaka Home: Mpangilio mzima na ratiba yako kwa siku umekaaje?
Chegge: Mara nyingi ninapokuwa bize na mazoezi ya kundi huwa naamka saa nne asubuhi, ninaporudi home nahitaji muda mwingi wa kukaa na kuandika nyimbo mpya, baadae najipunzisha.
Mpaka Home: Kwenye suala zima la kujiachia yaani kwenda katika sehemu mbalimbali za starehe kwako limekaaje?
Chegge: Hilo lipo, siku moja moja huwa machizi wangu wa kitaa wananipitia tunaenda kujichanganya maeneo mbalimbali.
Mpaka Home: Huwa unapenda kuandika mashairi wakati gani, ikiwemo kuingiza sauti studio?
Chegge: Mara nyingi huwa inategemea na mudi, kama ipo muda huo huo naandika, kuhusu kuingiza sauti (kurekodi) huwa inategemea na ratiba za studio.
Mpaka Home: Hivi sasa ukipata tatizo nani wa kwanza kumkimbilia?
Chegge: Mtu wa kwanza ni mama yangu mzazi kwa kuwa ndiye yuko karibu sana na mimi.
Mpaka Home: Unapendelea msosi wa aina gani?
Chegge: Kwenye suala la misosi huwa sichagui, wowote unaokubali kuingia kinywani huwa nakandamiza tu.
Mpaka Home: Unanufaika vipi na muziki wako hasa ukiwa kwenye kundi?
Chegge: Nanufaika na mambo mengi sana nikiwa ndani ya kundi ikiwemo kupata shoo nyingi ambazo naamini nikiwa peke yangu ni vigumu kuzipata.
Mpaka Home: Nini kauli yako kwa mashabiki wako na jamii nzima kwa ujumla?
Chegge: Wote kwa ujumla wakae mkao wa kula kusikiliza mipini yangu mipya ambayo itakuwa ndani ya albamu yangu ya tatu itakayokwenda kwa jina la ÔKaribu kiumeniÕ. Hivi karibuni nitaachia ngoma nyingine mpya itakayokwenda kwa jina la Mambo Bado ambayo nimemshirikisha Lady Jaydee.
Mpaka Home: Poa Chegge, pamoja sana.
Chegge: Nashukuru, karibu tena.
Friday, August 28, 2009
Posted in | |
0 Comments »
One Responses to "KUTANA NA MAISHA YA CHEGGE CHIGUNDA"