Ukiwa pande za Nanjilikitili halafu unasikia sifa za Bongo Records unaweza kudhani ni studio iliyopo kwenye eneo kubwa kama Kariakoo nzima.
Anayepunguza, basi ataamini ni go-down kubwa halafu ndani yake kuna mitambo ya nguvu, Mkurugenzi Mtendaji wake, Paul Matthysse ‘P. Funk’ analindwa na wapambe 50, ukithubutu kumsogelea umeumia.
Bongo Records ina jina kubwa. Ambao hawajawahi kuiona halafu wanaifikiria kwa ukubwa wa kupitiliza wana sababu ya kuifikiria kwa ukubwa huo.
Imewatoa wakongwe wengi tu, Juma Kassim Kiroboto ‘Nature’, Juma Mchopanga ‘Jay Moe’, Albert Mangwea ‘Ngwair’ na Jaffari Mshamu ‘Jaffarai’ na wengine wengi.
Mafanikio ya Joseph Haule ‘Prof. Jay’, Haroun Kahena ‘Inspector’ na Gangwe Mob, Wanaume Family na Halisi na utitiri wa wasanii wengi, kwa namna moja au nyingine, Bongo Records na mkono wa P. Funk ‘Kinywele Kimoja’ vimefanya waking’ara.
Tukumbuke kuwa kipindi kirefu Bongo Records ilibaki kuwa mtawala wa soko la Bongo Flava, ingawa kwa nyakati tofauti kulikuwa na ushindani na MJ Production ya Joachim Kimaryo ‘Master J’ na FM Studio wakati huo Mika Mwamba anasababisha.
Hata hivyo, kinachoonekana hapa ni kuwa P. Funk anashindwa kuiheshimu studio yake wala hajali ukubwa wa jina lake na ndiyo maana anakuwa na migogoro ya hapa pale na wasanii ambao wanakwenda kurekodi.
Ukiachana na vilio vya wasanii chipukizi, hata wakongwe nao imeonekana kasi yao ya kwenda studio hiyo imepungua. Kuna tatizo!
Ipo sifa inayoenea mtaani kwamba P. Funk ni master wa kusimamia vipaji, kwamba wale ambao hawawezi huwa haoni mbaya kuwatoa nishai. Hataki tu kuchukua pesa ya mtu, anaangalia kwanza kazi anayotengeneza. Anahitaji pongezi!
Hilo sawa lakini migogoro na wasanii wake ya nini? Mastaa wengi wanamuogopa kwa sababu dakika mbili mbele anaweza kubadilika na kufanya kitu cha kushangaza.
Ijumaa iliyopita, Mfalme wa Rhymes, Suleiman Msindi ‘Afande Sele’, alipita ofisini kwetu akiwa na furaha. Alikuja kutusabahi na baada ya hapo alitupa taarifa kwamba anakwenda Bongo Records kuchukua kazi yake kwa Majani.
Kwamba walikubaliana aende siku hiyo kazi yake ambayo Afande alirekodi na staa wa Ninao Ninao, Ferouz Mrisho Rehani.
Dakika 10 nyingi, Afande akawa anazungumzia Kituo cha Polisi kwamba amekwenda kumfungulia mashtaka P. Funk kuwa alimtukana, akampiga kofi na kumtishia bastola.
Hilo ni moja la Afande na hatuwezi kuingia ndani zaidi ya kesi hiyo kwa sababu kada za sheria zinazohusika zitafanya uamuzi lakini hapa tunatoa ushauri kiduchu kwa P. Funk.
Aheshimu studio yake kama kweli muziki ni kazi yake. Migogoro na wasanii hatakiwi kuipa nafasi, zaidi studio iwe sehemu ya heshima (ofisi), siyo eneo ambalo wakati wowote linaweza kugeuzwa ringi ya ngumi.
Pamoja na maoni haya, ntajaribu kucheki na Majani ili kujua nini hasa sababu ya kumchapa Afande ili kuweka usawa.
Monday, September 27, 2010
Posted in | |
0 Comments »
One Responses to "KOFI LA P-FUNK KWA AFANDE SELE"