Suma G
Dataz
Fleva ya ShowBiz ni safu ambayo nimeianzisha maalum kwa ajili ya kuangalia matatizo yaliyopo katika sanaa za Kibongo kama muziki, muvi na nyingine ambayo kwa kiasi fulani yamekuwa yakisabisha tasnia hizo ziendelee kupiga ‘maktaim’ hapa hapa TZ badala ya kuvuka mipaka na kwenda kimataifa zaidi. Utakuwa ukiipata hapa kila siku ya Ijumaa.
Tukija katika ishu yetu ya leo, tangu muziki wa kizazi kipya ulivyoanza kuota mizizi hapa Bongo na kuwa ajira kwa baadhi ya wasanii, vijana wengi wamejitokeza na kuonyesha vipaji vyao na kuifanya game hiyo iendelee kupokea wafanyakazi wengi zaidi kila kukicha huku wengine wakidiriki hata kujenga majumba na kumiliki aseti mbalimbali kupitia mradi huo wa ‘voko na biti’.
Lakini jambo la ajabu ambalo limekuwa likiwaacha watu wengi vinywa wazi ni juu ya mwenendo mzima wa sanaa hiyo na muziki huo ambao watoto wa mjini wameupa jina la Big G, yaani ngoma nzuri inapotoka inapendwa na mashabiki wengi na baada ya muda mchache inapotea, hata kama ikichezwa watu wanakuwa hawana ‘taimu nayo’.
Na siyo ngoma peke yake inayopotea, hata msanii aliyefanya kazi hiyo pia anapotea na inawezekana ukikutana naye miezi miwili baadae utamuhurumia kwa jinsi alivyochoka, utakapomuuliza jibu lake litakuwa “Nimeibiwa”. Wapo wasanii wengi wa muziki huo ambao pamoja na uwezo waliokuwa nao kwenye game wamepotea wala hakuna anayeuliza wako wapi.
Kila shabiki wa burudani hiyo anafahamu uwezo na ukali wa kuimba alionao Ferouz Mrisho ‘Ferouz’ ambaye tangu alipokuwa na kundi lake la Daz Nundaz alikuwa anakimbiza ukija kwenye ngoma yake, Starehe ndiyo balaa kwakuwa alionekana kuwa tishio kwa wasanii wengine kiasi kwamba walitamani kufanya naye kolabo ili kujiongezea nguvu kunako sanaa hiyo, lakini leo hii baadhi ya watu wameishamsahau.
Huu ni mfano tu wa wasanii wengi ambao thamani yao kwenye muziki imekuwa kama ‘Big G’ ambayo inakuwa na utamu pale unapoanza kuitafuna lakini baada ya muda hutapenda kuendelea kuwa nayo mdomoni. Wakati bado tukiendelea kutafuta mchawi wa hilo huku ikiwa halijafahamika tatizo ni nini hasa, shutuma nyingi zimekuwa zikirushwa kwa baadhi ya watangazaji wa vituo vya redio na televisheni wenye tabia ya kutanguliza pesa mbele bila kujali ubora wa kazi au kipaji cha kweli kabla ngoma hazijaenda hewani.
Lakini wasiwasi mwingine uliopo ni kuwa inawezekana uwezo mdogo wa kufikiri walionao baadhi ya wasanii katika kuandika mashairi yao na kutofanya utafiti wa kutosha ili kufahmu mashabiki wanahitaji kitu gani kwa wakati huo kabla ya kuingia kwenye sanaa hiyo vinanawafanya washindwe kutambua njia sahihi za kuwawezesha kubaki juu.
Pia wakati tunaendelea kurusha tuhuma hizo kwa watangazaji wasanii wetu pia wanatakiwa wajiulize mbali na muziki wao kuzimika kama ‘Big G’ kwanini hauvuki kwenda mbali zaidi, kwa mfano kuuza albamu Uingereza, Amerika na mataifa mengine ya Ulaya kama ilivyo kwa wenzetu Afrika Kusini, Nigeria, Congo, Uganda, Botswana, Senegal na nchi nyingine za Afrika?
Uchunguzi uliofanywa na ShowBiz umegundua kwamba, mbali na matatizo yote yanayotajwa bado kuna kila sababu kwa wasanii wetu kuumiza vichwa ili kutafuta aina ya muziki ambao utaenda mbali. Mashabiki wengi wamekuwa wakilalamika juu ya aina ya muziki ambao wasanii hao wanaufanya kuwa unaonekana kama ni wa kuiga badala ya wao kutafuta mtindo kutoka tamaduni za Kitanzania, jambo ambalo pengine lingewafanya kuwa juu kitaifa na kimataifa siku zote.
Huenda hili likawa jibu la moja kwa moja juu ya kile kinachowakuta wasanii wetu na kufananishwa na Big G, ni wazi kuwa mashabiki bado wana kiu kubwa ya kusikia kazi za kweli kutoka kwa akina Ferouz, Daz Baba, O-ten, Dataz, Pig Black, Crazy GK, Pico Kikongwe, Suma G, Mpaki, Mabaga Fresh, Sister P na wengine wengi katika kuusongesha muziki wetu.
Friday, October 8, 2010
Posted in | |
0 Comments »
One Responses to "MASTAA WETU NA THAMANI YA BIG G"