A.Y mmoja wa wakali wa muziki wa Bongo Flava wanaofanya muziki 'siriazi'
Bado tupo katika safari ya kuzifanya sanaa zetu za Bongo zipenye mbali zaidi a.k.a kimataifa, tunachotafuta hapa ni mchawi anayetufanya tuendelee kubaki tulipo badala ya kwenda mbali zaidi kama walivyo wenzetu wa nchi nyingine za Afrika. Ndiyo maana tukakuomba wewe msomaji na mdau wa burudani utusaidie kutuambia nini hasa kinasababisha kushuka kwa sanaa zetu.
Leo tunaicheki ishu moja ambayo kwa kiasi kikubwa inaunganishwa na sababu nyingine kibao zinazozifanya sanaa zetu zibaki kuishia hapa hapa nyumbani. Kuna mdau mmoja alinitumia meseji akionesha kusikitishwa kwake na baadhi ya wanasanaa wa Bongo ambao wakipata kujulikana kidogo wanajiweka juu zaidi kuliko jamii inavyowatazama, mimi kama mwanasanaa nikaona siyo mbaya nikiishusha hapa ili wewe msomaji na mpenzi wa burudani tuichangie kwa pamoja.
Kuna mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema kwamba umaarufu una nguvu ya ajabu na unaweza ukambadilisha mtu bila yeye kujijua, kitu ambacho nahisi kama kimeanza kuniingia akilini kwa sababu mimi ni mmoja kati ya watu waliopata bahati ya kuishi na baadhi ya watu ambao kabla hawajajulikana walikuwa tofauti na walivyo sasa. Wapo baadhi yao ambao hivi sasa wamekuwa ni walevi kupita kiasi na kusahau majukumu muhimu yaliyowaingiza kwenye sanaa zao.
Hawaishii kwenye ulevi wa pombe tu, kibaya zaidi hutumia hadi dawa za kulevya ambazo mwisho huwafanya waharibu kazi zao, ikiwemo kuwa na jeuri, kutoa maneno ya kashfa kwa jamii iliyowazunguka na kuwafanya wajulikane na inapotokea wakakosa ushirikiano kidogo kutoka kwa jamii hiyo kutokana na tabia zao hushindwa kuendelea na safari ya sanaa kisha hubaki wakijuta na kumuona kila mtu mbaya, wakati wamejiroga wao wenyewe na mwisho sanaa husika inaonekana haina maana tena.
Mbali na kundi hilo wapo baadhi ya wasanii wetu wanapopata kujulikana kidogo tu, inakua ni tiketi ya kuchukulia mademu au wanaume kwa ajili ya kufanya nao ngono tu na kusahau kwamba sanaa ni moja kati ya ajira muhimu ambayo wanatakiwa waiheshimu. Siku moja niliwahi kushikwa sikio na kuambiwa kwamba, kuna msanii mmoja wa kiume (jina ninalo) kila anapokwenda mikoani kufanya shoo baada ya kazi hulala na wasichana wawili au watatu kwa usiku moja, hebu tujiulize hiyo ndiyo maana ya umaarufu?
Kwa mifano hiyo michache inawezekana kabisa wapo baadhi ya wasanii wanaoingia kwenye tasnia hizo wakiwa hawajui wanakwenda kufanya nini au wakiwa na lengo moja tu la kutafuta majina ili wayatumie kufanya uzinzi na uasherati ikiwemo kwa wasanii wa kike kujiuza kwa mapedeshee ambapo mwisho wanawafanya hata wanaopiga kazi ‘siriasi’ waonekane wababaishaji. Ili tuzipeleke sanaa zetu mbele zaidi umefikia wakati sasa wa kuangalia nani ana nia ya dhati kutuinua na yupi anataka kutupeleka shimoni na tunapombaini tumuondoe kundini kwa kutompa ushirikiano.
Naamini mtu yeyote atakayeingia kwenye sanaa akiamini kwamba ndiyo kazi aliyoichagua kama ajira yake ya kudumu hawezi kutembea bega moja chini lingine juu au kutoa maneno ya kashfa mbele za watu pale anaposikika na wimbo mmoja tu redioni bali atakaa chini na kuumiza kichwa zaidi tena akisikia uchungu kwanini na yeye siku moja asipate mwaliko wa kwenda kufanya shoo Marekani kwa kina 50 Cent kama wao wanavyokuja Bongo. Vivyo hivyo kwa upande wa tasnia ya muvi siamini kama mtu huyo anaweza kujiita yeye ni supastaa kwa kushiriki kwenye filamu moja tu, tena akiwa amechezeshwa kama mhusika wa kazi na siyo ‘stelingi’.
Mwisho namaliza kwa kusema kwamba, wasanii wetu wanatakiwa kufahamu kuwa umaarufu siyo tiketi ya kufanya mambo maovu na kujiona wako juu ya jamii ambayo imewakubali kuwa vioo vyao, wanatakiwa wajione wao ni sawa na watu wengine kwa kushiriki kikamilifu kwenye matatizo ya kijamii pale wanapotakiwa kufanya hivyo inawezekana jamii hiyo ikawashauri na kuwapa mawazo mazuri yatakayowafanya wafike mbali zaidi badala ya kujiona wao ndiyo wao wakati hata ukienda kijijini kwetu ‘Nsemulwa’ hawajulikani. Tubadilike.
Friday, October 22, 2010
Posted in | |
0 Comments »
One Responses to "WASANII TUNAJUA MAANA YA UMAARUFU?"