Mabibi na mabwana leo katika stori ya Mpaka Home tunashuka na maisha ya msanii ‘first class’ katika game ya uigizaji wa filamu Bongo, si mwingine bali ni Jackline Wolper anayeishi pande za Kinondoni Studio, jijini Dar es Salaam.
Mpaka Home: Wasomaji wanataka kujua historia yako kwa kifupi.
Wolper: Jina langu halisi naitwa Jackline Wolper, nilizaliwa 1988 Moshi Kilimanjaro, chimbuko letu ni katika mkoa huo na kabila langu ni Mchaga, nimesoma Shule ya Msingi Mawenzi huko Kilimanjaro 1994-2000. Pia elimu ya sekondari nilianzia hapo hapo Mawenzi na baadaye nikaenda kumalizia Kenya 2001-2004.
Nilipohitimu nilirudi kwa wazazi ambapo sasa wanaishi Kibaha, Pwani na kipaji changu katika tasnia ya filamu kimeanza kuonekana mwaka 2008 jijini Dar es Salaam.
Mpaka Home: Changamoto zipi ulikutana nazo kabla ya umaarufu katika gemu?
Wolper: Ni nyingi, lakini moja ambayo ilikuwa kubwa kwangu ni kupata nafasi ya kuigiza, nakumbuka wakati huo malipo yalikuwa kiduchu sana.
Mpaka Home: Kuna filamu gani ambayo unaifanya wakati huu na mashabiki wako wategemee nini kutoka kwako?
Wolper: Kuna filamu ya Dar es Salaam Girls iko tayari ambayo ndiyo imemalizika hivi karibuni, nimefanya mambo makubwa katika filamu hiyo.
Mpaka Home: Unapenda chakula gani na unachukia nini?
Wolper: Napenda wali kuku, nachukia umbeya, lakini amani ndiyo kila kitu kwangu.
Mpaka Home: Ni msanii gani unayemkubali sana katika gemu hata kwa mwonekano wake?
Wolper: Kiukweli nawakubali sana akina Jenipha Mwaipaja (Shumileta), Zamda Salim na Irene Uwoya.
Mpaka Home: Mbali na filamu una mtazamo gani chanya kwa jamii inayokuzunguka?
Wolper: Mimi ni mjasiriamali, nimesaidia watu kibao ambao sipendi kuwataja hapa Bongo, lakini pia naelimisha jamii kupitia tasnia ya filamu.
Mpaka Home: Wasanii kibao wa Bongo huendekeza pombe,ngono na upungufu wa maadili, wewe unalizungumziaje hilo?
Wolper: Ni ulimbukeni na kuiga vitawamaliza kisanii, nawaomba wafanye kazi na waachane na mambo hayo.
Mpaka Home: Una mpenzi?
Wolper: Nina mchumba ila samahani siko tayari kumtaja.
Mpaka Home:Tanzania kuna vyuo vikuu vingi kipi ambacho unakipenda hata kwa kukisikia?
Wolper: Nakipenda sana Saint Augustine cha Mwanza, nawapenda wanaosomea uandishi wa habari ‘Mass-communication’maana nimewahi kutembelea maeneo hayo na kuna mdogo wangu anasoma pande hizo.
Mpaka Home: Unawaambia nini mashabiki wako?
Wolper: Wanipe sapoti.
Mpaka Home:Hili ni gheto lako la kujenga?
Wolper: Hapana hapa nimepanga ila nyumba yangu iko Mbezi Jogoo na ujenzi unaendelea ukiwa hatua za mwisho.
Mpaka Home:Vipi hapa ‘home’ majirani unaishi nao vizuri?
Wolper: Niko nao sawa, sijawahi kukwaruzana nao.
Mpaka Home:Unaizungumziaje tasnia ya filamu?
Wolper:Ni ngumu, yataka moyo.
Mpaka Home:Unaonekana kuwa na mvuto sana, vipi Mapedeshee hawakusumbui?
Wolper:Kama kawaida, wananisumbua sana hata kutaka kutumia hela zao na vitisho vya kunibamba, wengine wa hadhi za babu zangu huwezi amini, lakini najitahidi sana kuwalima vibuti.
Mpaka Home:Vipi ulishawahi kuachwa?
Wolper:Hapana ila nilishatema washkaji kama wawili hivi.
Mpaka Home: Wape neno la mwisho mashabiki wako.
Wolper: Nawapenda kwa kunisapoti.
Mpaka Home: Asante sana kwa ushirikiano wako.
Woper: Asanteni sana msela wangu big up! karibu tena.
Mpaka Home:Usijali nitakaribia.
One Responses to "MPAKA HOME KWA JAQUELINE WOLPER"